Alhamisi, 6 Machi 2014

MVUA KUBWA KUENDELEA UKANDA WA PWANI

“Hata shughuli za kilimo zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo.”Dk Agnes Kijazi.


DAR ES SALAAM.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetabiri kuwa mvua kubwa zitanyesha hasa maeneo ya ukanda wa pwani huku ikitahadharisha uwezekano mkubwa kusababisha maafa.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema jana kuwa utabiri huo unaonyesha kuwa maeneo mengi zaidi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani... “Hata shughuli za kilimo zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo.”


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari TMA pia imewahadharisha watumiaji wa bahari juu ya mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha bahari kuchafuka.


Taarifa hiyo imesema kunatarajiwa kuwapo kwa vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50, kati ya jana na kesho ambazo zitanyesha mfululizo na kwamba huenda zikasababisha madhara katika ukanda wote wa pwani.


Taarifa hiyo ilieleza kuwa mvua hizo zinasababishwa na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa Mashariki mwa Bahari ya Hindi, sanjari na kusogea haraka kwa mvua za masika hivyo kuongeza kiwango cha unyevunyevu kuelekea ukanda wa pwani.


Mikoa iliyopo katika ukanda huo ambayo inaweza kuathiriwa na mabadiliko hayo ya hali ya hewa ni Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar.


“TMA inazitaka mamlaka zinazohusiana na majanga kuchukua hadhari zinazostahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo,” ilisema taarifa hiyo.


Katika taarifa ya tathmini ya mvua za msimu kuanzia Machi hadi Mei, mwaka huu iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita, Mamlaka hiyo ilizitaka menejimenti za maafa na wadau wa sekta ya afya, kuchukua hatua za hadhari kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kutokea kwa kuwa baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani (TK)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni