Shirika la Afya Duniani linatarajia kutoa ushauri kuhusu dawa
inayoweza kutibu maradhi ya Ebola baadaye leo Mjini Geneva kufuatia kikao cha
siku mbili cha wataalam wa udhibiti wa magonjwa , watafiti wa tiba, makampuni
ya madawa na nchi waathirika .
Hakuna chanjo wala tiba inayofahamika kwa mlipuko wa sasa wa Ebola ambao ni
mbaya zaidi kuwahi kuukumba ulimwengu , ukiwaua watu wapatao 2000 . Bado ugonjwa huo unaripotiwa katika nchi sita za Afrika .Haja ya kubaini aina fulani ya tiba ya ugonjwa huu ni ya dharura. Virusi vya Ebola vinaonekana kuenea kupita kiasi cha uwezo wa kuvidhibiti, huku vifo 400 vinavyotokana na maradhi hayo vikiripotiwa wiki iliyopita pekee.
Mifumo ya afya katika nchi zilizoathiriwa Liberia, Guinea,na Sierra Leone inakaribia kukosa kabisa uwezo wa kutoa huduma za matibabu.
Magonjwa mengine hatari kama Malaria hayataweza kutibiwa. Lakini hata kama mkutano huu utabaini dawa mpya za kukabili maambukizi haya, hazitakuwa tayari kutumiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Wakati huo huo virusi vya Ebola vinaendelea kusambaa, na baadhi ya wanasayansi wanahofu ya kubadilika kwa aina ya virusi hiyo. Mkakati pekee kwa Ebola ni kuudhibiti, lakini juhudi zilizopo kwa sasa hazionekani kufua dafu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni