Kamati za
Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 27 Aprili hadi tarehe 4 Mei
2015 Jijini Dar es Salaam, kutekeleza Majukumu yake, kabla ya Mkutano wa
Bunge wa Bajeti uliopangwa kuanza mjini Dodoma tarehe 12 Mei na kudumu
hadi tarehe 25 Juni, 2015. Kwa kawaida, Kamati za Kudumu za Bunge
hupaswa hukutana wiki mbili kabla ya Mkutano wa Bunge, ama Dar es
Salaam, Dodoma au Zanzibar kuendana na matakwa ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la Aprili 2013.
Hivyo,
Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo
Jumapili tarehe 26 Aprili 2015 tayari kwa kuanza vikao siku ya Jumatatu
tarehe 27 Aprili, 2015.
katika vikao hivyo Kamati 13 za Bunge zitajadili utekelezaji wa
Bajeti ya Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi kwa mwaka
2014/2015 na mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2015/2016.
Siku ya
Jumatano tarehe 28 Aprili, 2015 Wabunge wote kwa ujumla wao watakutana
katika Ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere kupokea Mapendekezo ya Mpango,
Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali ya 2015/2016 kwa mujibu ya
matakwa ya Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2013.
Baada ya shughuli hiyo, Kamati zote za Kisekta zitaendelea na uchambuzi
wa Bajeti kuanzia tarehe 29 Aprili hadi 8 Mei, 2015.
Pamoja na
hayo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali itatumia muda huo kujadili
Hesabu za Mikoa zilizokaguliwa zinazoishia tarehe 30 Juni, 2013 na
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa itafanya ziara za ukaguzi
wa thamani kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa mwaka wa fedha
unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 katika mikoa ya Dodoma na Singida.
Tofauti na kamati nyingine, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa imeanza kazi zake mapema tarehe 20 Aprili, 2015 ambapo inajadili
Bajeti za Mikoa ya Tanzania Bara na Bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2015/2016.
3.0 SHUGHULI NYINGINE
Shughuli za Kamati zitamalizika tarehe 8 Mei, 2015 Jijini Dar es
Salaam ambapo Mkutano wa Bunge wa Bajeti utaanza tarehe 12 Mei, 2015
Mjini Dodoma na unategemewa kumalizika tarehe 25Juni, 2015. Ratiba za
shughuli za Kamati zote zitapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni
www.parliament.go.tz
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
22 Aprili 2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni