Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alisema jana kuwa Sarah
alifariki dunia juzi saa moja jioni, katika Hospitali ya Wilaya ya
Njombe ya Kibena, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.
Alisema mkuu huyo wa wilaya aliugua ghafla juzi muda mfupi baada ya
kutoka ofisini na alianza kujisikia vibaya alipokuwa akijiandaa kula
chakula alichokuwa ameandaliwa.
“Mkuu wa wilaya alipofika nyumbani kwake, alitaka kupata chakula
lakini alianza kupata shida ya kupumua na baadaye kuanza kulegea mwili.
Alipelekwa katika Hospitali ya Kibena ndipo umauti ukamfika akipatiwa
matibabu,” alisema Dk. Nchimbi
Dk. Nchimbi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali
Teule ya Wilaya ya Wanging’ombe ya Ilembula, ambayo ndiyo ina uwezo wa
kuhifadhi maiti.
Alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na kwamba leo
kutakuwa na ibada maalum ya kuaga mwili wake katika Kanisa Kuu la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini mjini hapa,
alikokuwa akiabudu.
Mkuu wa Mkoa alisema baada ya hapo, mwili wa marehemu utasafirishwa
kwenda Dar es Salaam, ambako familia yake inaishi maeneo ya Kigamboni,
kwa maziko ambayo yatafanyika siku ya Alhamisi tarehe 24/3/2016.
Sarah alianza kazi ya ukuu wa wilaya mwaka 2006 katika wilaya ya
Kilindi mkoani Tangana baadaye kuhamia Njombe (wakati huo ikiwa katika
mkoa wa Iringa) na sasa mkoa wa Njombe, alikotumika hadi kufariki dunia.