NINAPOFIKA nyumbani kwa Jackson Ngowo, eneo la Goba, kilomita tisa 
kutoka Mbezi Tangibovu, Dar es Salaam na kupokewa na wenyeji wangu, moja
 kwa moja napelekwa katika chumba alicholala mtoto Wilson mwenye umri wa
 miaka 11.
 
Ninamkuta Wilson akiwa amelala kwenye godoro. Anageuza shingo 
taratibu kuniangalia. Ninapo mwita na kumsalimia nikitaka kujua 
anaendeleaje, Wilson anaishia kuguna na kutikisa kichwa kwa shida, ikiwa
 ni ishara ya kuitikia salamu yangu.
Hilo tu linathibitisha mateso ya takribani miezi sita ambayo amekuwa 
akiyapata mtoto huyu, na muda wote huo akiwa mtu wa kitandani kinyume na
 watoto wenzake huko nje wanaokwenda, shule, kusoma na kucheza ambao 
miezi sita iliyopita alikuwa akijumuika nao pamoja. Pembeni mwa godoro 
alilolalia Wilson, amelala mama yake aitwaye Neema.
Mama huyu anasema amelala pale kutokana na shinikizo la damu (pressure) linalomsumbua.
"Tangu jana nasumbuliwa na presha," anasema Neema akiwa ameketi 
kwenye godoro, kando ya mwanawe. Maneno machache yanayoweza kumwelezea 
kwa kifupi mtoto Wilson ni kwamba hawezi kuamka kitandani, hajigeuzi na 
hata matumaini ya kurejea shuleni sasa kwake yanaonekana kama miujiza.
Kilichomfanya mtoto huyu awe hivyo ni ajali. Masimulizi yanaonesha 
kwamba siku ya tukio, Wilson akiwa amepakiwa kwenye pikipiki, waligongwa
 na gari ina ya Fuso katika eneo la Mpiji Magowe.
Mbali na kuvunjika mguu, mtoto huyo wa nne kati ya watoto sita wa 
Jackson Ngowo, alipata pia matatizo kwenye kichwa na ubongo kutokana na 
ajali hiyo.
Ufafanuzi zaidi wa wazazi wake wakimkariri daktari wa mtoto huyo na 
vipimo vya X-ray unaonesha kwamba mishipa inayounganisha kichwa na uti 
wake wa mgogo iliathiriwa na hivyo kuathiri pia uwezo wake wa kutoa 
sauti.
Kwa mujibu wa wataalamu (angalia katika www.asha.org), Wilson atakuwa
 pia anasumbuliwa na tatizo linaloitwa kwa Kiingereza aphasia 
linalomfanya ashindwe kuzungumza. Hii ni hali ya mtu kushindwa kuongea 
kutokana na sehemu ya ubongo wake, hususani nusu ya ubongo wa sehemu ya 
kushoto, kupata majeraha.
Mtandao huo pia unaonesha kwamba mtu mwenye aphasia, mbali na 
kushindwa kuongea, anaweza pia kushindwa kusikia, kusoma na kuandika 
lakini hilo haliathiri uwezo wake kiakili (intelligence).
Wilson kila mara anaonekana mwenye huzuni hata pale anapotaka 
kuonesha kufurahia wageni wanaomtembelea. Baada ya kuniona, kwa mfano, 
alionesha hali ya kutaka kutabasamu, lakini ikawa ngumu kwake kutokana 
na hali aliyonayo.
Mtoto huyu, kwa sasa anahitaji nepi maalumu aina ya pampas, anahitaji
 lishe na kubwa zaidi ni matibabu ili aweze kurudi katika hali yake ya 
kawaida au hata kama hatafikia kwa asilimia 100 basi amudu kujisaidia 
mwenyewe.
Mkasa wenyewe Masimulizi ya wazazi wake yanaonesha kwamba ilikuwa 
Jumapili ya Februari 28 mwaka huu, siku iliyobadili utaratibu na ugumu 
wa maisha wa familia ya Jackson Ngowo na mkewe, Neema Ndosi, pale watoto
 wao wawili walipopata ajali ya kugongwa na Fuso.
Siku hiyo, baba yao (Jackson) ambaye ni fundi mwashi, aliwatuma 
wanawe hao, Ibrahim na Wilson kwenda kwenye kibanda cha kutolea pesa ili
 kumletea fedha taslimu alizokuwa anazihitaji kutoka kwenye simu yake.
“Nilikuwa nimewatuma kutoa fedha kwenye simu. Walipoona kile kibanda 
nilichowatuma kimefungwa walikwenda kibanda cha mbele zaidi na wakaomba 
kijana wa jirani awapakize kwenye pikipiki, ndipo walipogongwa na Fuso, 
anasema Ngowo ambaye sasa anaishi Goba alikosaidiwa kupanga vyumba 
viwili. Anaongeza: “Baada ya wanangu kupata ajali, nilipigiwa simu kuwa 
mwanao mmoja amefariki dunia (Wilson) na mwingine hali ni mbaya 
(Ibrahim)."
Anasema aliwakimbiza watoto wake hao wawili kwenye hospitali ya 
Tumbi, Kibaha baada ya kugundua kwamba hata Wilson alikuwa hajafa.
Anasema kutokana na hali yake, baadaye Wilson alihamishiwa kwenye 
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako alilazwa kwenye chumba cha 
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa miezi mwili na siku 
tisa.
“Hali imekuwa ngumu kwangu kwa miezi sita yote ya kuuguza wanangu 
wawili. Mmoja alikuwa amelazwa Tumbi, Kibaha na mwingine ICU, Muhimbili 
kwa miezi miwili na siku tisa,” anasema.
Kama ilivyo kawaida kwa ajali nyingi, Ngowo anasimulia kwamba Fuso 
lililosababisha ajali hiyo na kukatisha ghafla furaha na ustawi wa 
Wilson lilikimbia na hawakuweza kulitambua.
Mama wa watoto hao, Neema anasema wamehangaika sana kuokoa maisha ya 
watoto wao na hivyo anawashukuru majirani na wasamaria waliowasaidia 
hadi kufikia hapo. Hata hivyo, anasema hali bado imekuwa nzito katika 
kuwauguza watoto wao, hasa Wilson kutokana na gharama nyingi kuhitajika 
kulinganisha na uwezo wao.
“Tulilazimika kuuza makochi, vitanda na magodoro, nguo na vitu vidogo vidogo ili kuweza kugharamia matibabu ya watoto wetu.
“Hata haya magodoro tuliyonayo sasa tumepewa na wasamaria wema na 
hata vyumba hivi viwili tulivyopanga ni hisani ya watu," anasema. Ngowo 
anaomba watanzania kusaidia matibabu ya mtoto wake Wilson.
“Nashukuru Mungu kwa Ibrahim afya yake imetengamaa lakini kwa Wilson 
hali bado ni mbaya kwani ni mtu wa kujisaidia kila kitu na hajaweza 
kurejea katika hali ya kawaida,” anasema.
Ngowo anasema gharama za matibabu ya mtoto wake ambaye sasa anamtibu 
katika hospitali ya Profesa William Matuja iliyopo Upanga ni wastani wa 
Sh 200,000 hadi Sh 400,000 kwa mwezi, na kwamba matibabu hayo yanatakiwa
 kuchukua zaidi ya mwaka mmoja.
“Tuliporuhusiwa MOI, hali ya mtoto haikuwa si ya kuridhisha kabisa, 
tuliruhusiwa tukiwa bado tunamlisha kwa mipira, lakini baada ya 
kumpeleka kwa Profesa Matuja, ndio unafuu ambao kwa sasa tunaona kwa 
mwanetu. Sasa anaweza hata kuguna unapowasiliana naye,” anasema Ngowo.
Ukiachia gharama za matibabu ambazo ni kumuona daktari na dawa, 
lakini pia Wilson anatakiwa kufanyiwa usafi wa kidonda kila baada ya 
siku mbili au tatu, matibabu yanayogharimu zaidi ya Sh 22,000 pamoja na 
usafiri.
“Kwa hali yake, huwezi kumsafirisha kwa bodaboda wala bajaji, hivyo 
tunalazimika kutumia gari ili aweze kulazwa kwenye kiti, jambo ambalo 
linachangia gharama hiyo," anasema. Anasema kilichobainishwa na daktari 
ni kuwa misuli inayounganishwa kichwa na uti wa mgongo ndiyo 
iliyoathirika sambamba na mfumo wa sauti ingawa uti wa mgongo haujapata 
matatizo.
Ngowo anasema alipewa barua ya kutakiwa kwenda hospitali ya Jeshi ya 
Lugalo kwa ajili ya kumfanyia mazoezi ya misuli lakini huko akajibiwa 
kuwa hospitali hiyo inaweza kumfanyisha mazoezi tu mtoto ambaye anaweza 
kutembea au kujitegemea. Anasema huko walimtaka ampeleke katika 
hospitali ya Mbweni ambayo gharama yake ni Sh 25,000 kila anapofanywa 
mazoezi.
Anasema wapo hata waliomwambia tatizo la Wilson, linaweza kutibiwa 
kirahisi nje ya nchi, hususani India, lakini hilo hataki kulifanyia kazi
 kwa sasa kwani ni 'mlima mkubwa' kwake kama tu matibabu ya hapa ndani 
inakuwa shida.
“Kusema ukweli nimekwama kabisa ndio maana nimekuja kwenu, ili 
kupitia ninyi (waandishi wa habari) niwaombe watanzania wanisaidie 
kunusuru maisha ya mwanangu. Natamani arudi tena shule na kuendelea na 
masomo,” anasema.
Anaongeza: “Hata tuliporuhusiwa kutoka Moi nilikuwa na deni la zaidi 
ya laki saba, ambalo wasamaria wema ndio walionisaidia kulilipa."
Kutokana na hali ya maisha ya familia yake, hata suala la lishe kwa 
mtoto huyo bado linaonekana gumu, jambo ambalo linazidi kudhoofisha 
mwili wa Wilson na hivyo kuchelewesha uponyaji kwake.
Neema anasema kwa mujibu wa maelekezo ya daktari mtoto huyo anatakiwa
 kunywa lita moja ya maziwa kila siku, uji wa lishe na samaki 
aliyechemshwa na supu ya mboga, vyakula ambavyo vitamsaidia pia katika 
kupona haraka.
“Kutokana na hali yetu hakuna hata tunachokifuata. Tumekuwa 
tukimlisha chochote kinachopatikana, hasa uji pale tunapojaliwa kupata 
fedha,” anasema huku akiwa anamlisha uji wa sembe unaoaminika kwamba 
hauna virutubisho vya muhimu mwilini kwani unatokana na unga wa kukoboa.
Aidha, Ngowo pia anaomba jamii ya watanzania imesaidie kupata kiti 
cha magurudumu kitakachosaidia kumkalisha mtoto huyo ili kunyoosha 
viungo, tofauti na sasa ambapo muda mwingi amekuwa akilala.
“Muda mwingi amekuwa akilala, mara moja moja namtoa nje kwa kumbeba 
ili aote jua, maana daktari alituelekeza kuhakikisha tunamtoa nje,” 
anasema Neema.
Anaongeza: “Hata wakati wa kumsafisha inakuwa shida. Ni lazima 
nimvute mbele na kisha nimgeuze taratibu upande mmoja na upande 
mwingine, hali ambayo inamuongezea maumivu." Familia ya Ngowo inaomba 
msaada wa hali na mali ili kusaidia matibabu ya mtoto wao Wilson 
Jackson.
Mnaombwa msaada kupitia simu namba 0652 255 942 (Jackson Ngowo) au 
0742 731 878 (Neema Ndosi). Aliyeguswa pia anaweza pia kumchangia 
chochote mtoto huyu kupitia Mhariri wa gazeti la Habari leo 0766 843 3