WAFANYABIASHARA wawili, Harbinder Sethi na James Rugemalira
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam kwa mara ya pili na kusomewa mashitaka mapya sita likiwamo la
utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Kimarekani milioni
22.1 na Sh bilioni 309.4.
Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering na
mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power
Tanzania Ltd (IPTL) na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya
Power African Power (T) Limited (PAP), walisomewa mashitaka hayo jana
mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi, yakifanya sasa wakabiliwe na
mashitaka 12 baada ya awali kupandishwa kizimbani Juni 19, mwaka huu,
ambako walikabiliwa na mashitaka sita.
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro alidai
washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na
mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha
kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha
fedha. Kimaro alidai kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini
Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na
India ili kutenda kosa.
Alidai katika mashitaka ya pili kati ya Oktoba 8, 2011 na Machi
19,2014 jijini Dar es Salaam, wakiwa siyo watumishi wa umma
walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mtandao huo wa uhalifu
kwa lengo la kujipatia faida.
Katika mashitaka ya tatu yanayomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba
10, 2011 katika Mtaa wa Ohio Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam
akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni
na kuonesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa
Mrikau, Masaki wakati akijua sio kweli.
Pia Sethi anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14
A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa
njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau,
Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Kimaro alidai katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati
ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao Makuu ya Benki
ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi, Tawi la Mtakatifu Joseph,
kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania
(BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Shilingi za Tanzania 309,
461,300,158.27.
Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo
inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic,
Tawi la Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya
Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kimaro alidai kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo
tofauti Dar es Salaam, kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha
kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na
Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na
genge la uhalifu.
Katika mashitaka ya nane, Kimaro alidai kuwa Novemba 29, 2013 katika
Tawi la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi
alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BOT dola za Marekani milioni 22.1
wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la
uhalifu.
Aidha, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014
katika Tawi la Benki ya Stanbic Kinondoni, Dar es Salaam alitakatisha
fedha Sh bilioni 309.4 kutoka Benki Kuu ya Tanzania wakati akijua fedha
hizo zimetokana na zao uhalifu.
Katika mashitaka ya 10, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya
Mkombozi, Tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalira alitakatisha fedha
ambazo ni Sh bilioni 73.5 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo
zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Pia inadaiwa Januari 23, 2014 katika tawi hilo la Benki ya Mkombozi,
Rugemalira alitakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani milioni 22
kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.
Kimaro pia alidai Sethi anadaiwa kuwa Januari 28, 2014 katika Tawi la
Benki ya Stanbic, Kinondoni alihamisha Rand za Afrika Kusini 1,305,800
kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land
Rover Sandton ya Afrika Kusini wakati akijua katika kipindi anahamisha
fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo
haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Hata hivyo, upande
wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na
washitakiwa wamerudishwa rumande hadi Julai 14, mwaka huu kwa kuwa
mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao hayana
dhamana.