Jumatano, 16 Aprili 2014

MAFURIKO DAR WATU 25 WAFARIKI

Mafuriko Dar es Salaam, Tanzania

Watu 25 wamethibitika kufa mkoani Dar es Salaam nchini Tanzania kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo kuanzia Ijumaa hadi Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo akisema watu wengine 14 wanadaiwa kufa, lakini hawajathibitishwa na polisi.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam wenye wilaya tatu, amesema watu 11 wamekufa katika wilaya ya Ilala, huku wengine wawili hawajaonekana mpaka sasa.

Taarifa kutoka wilaya ya Temeke imesema watu saba wamethibitishwa kufa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha.

Pia kuna taarifa za watu 21 kufariki dunia katika wilaya ya Kinondoni, japo hawajathibitishwa.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Sadik amesema miundombinu ya barabara na madaraja imeanza kurejeshwa baada ya kuharibiwa na mafuriko na kusababisha mkoa wa Dar es Salaam kukosa mawasiliano ya ndani na pia kukosa mawasiliano na mikoa jirani. (TK)

WAASI WA SUDAN KUSINI WAUTEKA MJI WA BENTIU

 
Waasi wadai kuudhibiti upya Bentiu kutoka kikosi cha serikali

Wapiganaji nchini Sudan Kusini wanasema wameudhibiti mji mkubwa katika jimbo lenye utajiri wa mafuta, na wametoa makatazo kwa makampuni ya mafuta kusitisha uchimbaji wa mafuta na iwaondoshe wafanyakazi.

Walinda amani wa Umoja wa mataifa waliwaokoa wafanyakazi kumi wa kampuni ya mafuta ya Urusi, Safinat kaskazini mwa mji wa Bentiu, kutoka ghasia hizo, watano kati yao walijeruhiwa.

Sudan kuisni imeshuhudia ghasia kubwa mnamo mwezi Desemba, wakati kulizuka mapigano kati ya wanajeshi wanaomtii aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar na wale wanaomtii rais Salva Kiir.

Maelfu ya watu wanaaminika kuuawa huku wengine zaidi ya milioni wakiyakimbia makaazi yao.

Raia wengi wametoroka makaazi yao kutokana na mapigano

Wakati mapigano hayo yanaendelea mratibu wa misaada wa Umoja wamataifa nchini humo, Toby Lanzer, ameghadhabishwa na kukasirishwa na viongozi wa kisiasa na kijeshi Sudan kusini.

Amesema kuzuka upya mapigano hayo kutaathiri jitihda za kuepuka baa la njaa linalotarajiwa.

Maafisa wa mashirika ya kimataifa ya misaada wametumia 'baa la njaa' mara kwa mara kuelezea hali itakayoikabili Sudan kusini katika miezi ijayo.

Nchi hiyo ni maskini na wakazi wengi wanaishi kwa kula vyakula wanavyopanda na kuvuna. Kutokana na mapigano yanayoendelea, wakazi wengi wanashindwa kupanda vyakula kwa matayarisho ya msimu ujao wa mvua (TK).

Wanafunzi wa kike watekwa nyara Nigeria

Polisi nchini Nigeria wanasema kuwa shule ya mabweni ya wasichana imeshambuliwa katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo huku wasichana wakitekwa nyara.

Shambulizi hili linadaiwa kufanywa na Boko Haram ingawa kundi hilo halijakiri kulitekeleza

Wazazi wanasema kuwa zaidi ya wasichana mia moja wametekwa nyara na washambuliaji hao.



Washambuliaji wanaaminika kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram. Utekaji nyara huo ulifanyika usiku wa manane katika shule ya Chibok Kusini mwa mji wa Borno, karibu na mpaka na Cameroon.

Inaarifiwa wasichana 300 walikuwa wanajiandaa kwa mitihani yao. Mmoja wa wasichana alifanikiwa kutoroka na aliambia BBC kuwa walikuwa wanalala wakati walipovamiwa na wanaume waliokuwa wamejihami.

Waliowashambulia wanaaminika kuwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Wanaume hao waliingiza magunia ya chakula katika malori yao na kuwaamuru wasichana kupanda lori hizo.

Wasichana 15 walifanikiwa kutoroka baada ya lori walimokuwa kukumbwa na hitilafu.

Wakazi wa kijiji cha Chibok wanasema kuwa walisikia milipuko kadhaa huku nyumba 170 zikiteketezwa.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa wanajeshi wawili waliuawa huku mali ikiharibiwa wakati wa shamblizi hilo mjini Chibok.

Mnamo siku ya Jumatatu, zaidi ya watu 70, waliuawa katika milipuko miwili ya mabomu katika kituo cha mabasi mjini Abuja.

Kundi la Boko Haram pia limelaumiwa kwa kufanya shambulizi hilo (TK)

MHIFADHI MKUU VIRUNGA NP APIGWA RISASI DRC

Sokwe hawa wa milimani wanakabiliwa na tisho la kutoweka kutokana na kuwindwa sana

Mmoja wa viongozi wakuu wa uhifadhi wa wanyama pori barani Afrika Emmanuel de Merode, amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika moja ya mbuga kongwe barani afrika.

Bwana Merode,ambaye ni raia wa Ubelgiji ni mkurugenzi wa mbunga ya wanyamapori ya Virunga, ambayo ni makao ya Sokwe wanaokaa milimani katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Sokwe hao ni baadhi ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka kutokana na kuwindwa sana.

Alipigwa risasi akiwa anaendesha gari kati ya eneo lililo kati ya makao makuu ya mbuga hiyo na mji wa Goma ambako amelazwa hospitalini.

Sababu ya kupigwa risasi kwa mhifadhi huyo haijajulikana, lakini makundi ya watu ambao hukata miti kiharamu, wawindaji haramu na waasi huendesha shughuli zao katika eneo hilo -BBC (TK)

MELI (FERRY) YA KOREA YA KUSINI YAZAMA


Watu walionusurika wamekuwa wakielezea hali ilivyokuwa ya kutisha ndani ya meli ya Korea Kusini ilipoanza kusimama kwa kuyumba, akiegemea upande mmoja na haraka kuanza kuzama.

"Kwa kweli kulikuwa na sauti kubwa na meli ghafla ikanza kuegemea upande mmoja," amesema abiria aliyeokolewa, Kim Song-Muk.

Meli ya Korea Kusini ikizama kulia

"watu walikuwa wakihangaika kukimbilia maeneo ya juu ya meli, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na meli kupinduka."

Bado haijafahamika kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa iliwabeba wanafunzi wa shule, lakini watu walionusurika katika ajali hiyo wanatoa maelezo sawa kuhusu tukio hilo la kutisha.

Kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Korea Kusini kimesema abiria wapatao mia tatu hawajulikani walipo baada ya meli kupinduka na kuzama.

Mtu mmoja wamethibitika kupoteza maisha na watu mia moja na sitini na wanne wameokolewa. Kikosi cha wapiga mbizi kwa sasa wanatafuta meli iliyozama. Wengi wa abiria wa meli hiyo ni wanafunzi wa sekondari wakiwa katika safari ya masomo kuelekea kisiwa cha Jeju, nchini Korea Kusini.

Meli hiyo ilikuwa na watu 460

HOJA 12 ZA MHE MBILINYI

Screen Shot 2014-04-15 at 12.24.52 PM

Wajumbe mbalimbali kwenye bunge la katiba wameendelea kuwasha vipaza sauti vyao kuchangia, kutoa ya moyoni kwa kujadili sura ya kwanza na ya sita huku ishu ya serikali mbili au tatu ikizimiliki headlines zaidi.
Zifuatazo ni kauli za mjumbe Mh. Joseph Mbilinyi ambaye pia ni mbunge wa Mbeya mjini April 15 2014
1. ‘Wabunge Wakristo hii ni kwaresma, ni kipindi cha toba… mnatumia kipindi hiki kufanya unafiki mbele ya Wananchi mtakuja kuhukumiwa siku itakapofika, wameharibu mchakato wakati tumeshatumia mabilioni mengi ya hela’
2. ‘Ukarabati tu wa jengo la bunge hili ili sisi tukae zimetumika BILIONI 8.2 halafu leo kwa sababu ya hotuba moja tu ya Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wote wamegeuka, wanaharibu kabisa tunashindwa kufanya mambo ya maana, wanaacha kupanga mkakati wa hoja wanapanga mkakati wa kuzomea, wameishiwa mikakati mpaka wanazomea kimkakati’
3. ‘Unakutana na mbunge tena Waziri kama rafiki yangu Mwigulu Nchemba tunataniana ananiita mzee wa Maandamano mi namuita mzee wa kuteka, ananiambia wewe Sugu sijui unataka serikali tatu sijui vipi na vipi, namwambia kwani hutaki kabisa Tanganyika anasema mi nataka Tanganyika ila nataka serikali moja, sasa kama mnataka serikali moja kwa nini uibuke kwenye hoja ya serikali mbili?

4. ‘Kuna watu ambao wanajadili vitu ambavyo hawaviamini na havipo kwenye mioyo yao na hao watu wana dhamana kwenye uongozi wa taifa hili na hii ni hatari’

5. ‘Tuko kwenye nafasi nzuri sana ya kujadili hili suala, tulijadili wakati tunaheshimiana kuliko siku tuje kulazimisha mabadiliko ambayo hatukuyapanga, tusifikie sehemu Wazanzibari hao wanaosemwa elfu sitini ndio waingie barabarani na jeshi’
6. ‘Mwenyekiti alikuja hapa akatutisha oooh sijui serikali tatu, Mwanajeshi atakuja atachukua nchi… Mwenyekiti mwenyewe alikuwa ni Mwanajeshi akavua uniform, Nyerere aliposema vueni uniform akavua na leo ni rais, kuna ubaya gani Mwanajeshi akitawala kama ana akili? hakuna ubaya, wanajeshi ni ndugu zetu’
7. ‘Hakuna tatizo lolote siku Mwanajeshi akija kuwa Rais kwa sababu tunae Mwanajeshi Rais Kikwete na anaendelea tu, asiweke vikwazo kwa Wanajeshi wengine ambao watakuwa na tija kwa taifa hili’
8. ‘Wanasema serikali tatu gharama, hivi kama gharama inaongezeka halafu tija inaongezeka kuna tatizo gani? ukifanya biashara rejareja ukitaka kuwa mkubwa ni lazima uongeze mtaji, kama huu mfumo wa serikali mbili umeshindwa kutuondolea matatizo mwengine anasema Znz wana hiki wana kile, mbona hamsemi kama mpaka umeme tunawalipia?? lakini sisi huku tunalia’

9. ‘Tuna serikali mbili na hakuna alieysimama hapa akasema serikali mbili gharama zake zipi, Wizara ngapi hapa zinapanga majengo kila siku yanatolewa furniture? serikali tatu gharama against what? against tija? against maendeleo? against kwenda mbele?
10. ‘Sababu akili yenu ni fedha ndio maana mnaangalia faida kwamba ni fedha tu, hamuangalii faida nyingine za kijamii ambazo zitaleta tija kwa taifa hili’
11. ‘Kuna hawa ndugu zangu viongozi wa dini, tunasema hivi mara nyingi viongozi wa dini wamekosea walipochagua kuwa upande wa dola dhidi ya matakwa ya nchi, hii imetokea mfano ni Padri wa Rwanda, leo hii yuko wapi? kwa hiyo viongozi wa dini wawe makini wanavyoangalia haya maswala’

MATUMAINI YA ARSENAL KUCHEZA UEFA YAFUFUKA


MATUMAINI ya Arsenal kufuzu kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao yameanza kufufuka baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham kwenye mchezo wa ligi kuu soka nchini England uwanja wa Emirates.
Lukas Podolski amefunga mabao mawili katika dakika ya 44 na 78, huku moja likifungwa na Olvier Giroud dakika ya 54.
Westham walikuwa wa kwanza kufunga leo hii katika dakika ya 40 kipindi cha kwanza kupitia kwa Matthew Jarvis .
Mashabiki wa Arsenal huwa hawana imani kubwa na Giroud na katika mchezo wa leo alikosa nafasi kadhaa kipindi cha kwanza, lakini wakati mashabiki wakijiuliza kama mshambuliaji huyo anaweza kuwa tegemeo kwa siku za usoni, alifunga bao muhimu mno katika ushindi huo.
Umuhimu wa bao la Giroud unatokana na uhitaji mkubwa wa Arsenal kufuzu michuano ya UEFA msimu ujao.
Kikosi hicho cha Arsene Wenger kilianza vizuri ligi na kuongoza kwa muda mrefu, lakini mambo yakabadilika ghafla na kuwapisha Chelsea, Man City na Liverpool ambao wanachuana mpaka sasa.
Sasa Wenger na vijana wake wapo katika hatari ya kushindwa kufuzu UEFA kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 17 baada ya kuwapisha Everton katika nafasi ya nne kwa muda.
Lakini baada ya kushinda mechi ya leo dhidi ya wapinzani wao wa London, Arsenal wamerejea nafasi ya nne kwa kufikisha pointi 67, huku Everton wakishuka mpaka nafasi ya tano kwa pointi zao 66, lakini kesho wanacheza dhidi ya Crystal Palace.
Arsene Wenger baada ya mchezo amesema kuwa walikuwa katika presha kubwa ya kushinda mchezo, lakini ilikuwa mechi ngumu mno.
“Niliridhishwa na ukomavu wa timu yangu. Walionesha kutulia baada ya kufungwa bao la kwanza”.


“Kazi kubwa ilikuwa kusawazisha bao kabla ya mapumziko. Ilikuwa vita kubwa na ilikuwa ya kufurahisha”. Alisema Wenger (TK)

Jumanne, 15 Aprili 2014

Mke wa Rais wa Kenya aweka historia London


Bi Kenyatta akilakiwa na mumewe Rais Uhuru Kenyatta

Mama Margaret Kenyatta mke wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, amekuwa mwanamke wa kwanza mama wa taifa kushiriki mbio za London Marathon na kumaliza mbio hizo.

Alishangiliwa na wakenya wanaoishi nchini Uingereza alipomaliza mbio hizo za kilomita 42 kwa muda wa saa saba na dakika nne siku ya Jumapili.

Mama Margaret alilakiwa na Rais Kenyatta pamoja na waandalizi wa mbio hizo mjini London mwishoni mwa mbio huku akiwapa motisha wakenya na jamii ya kimataifa kwa kuwa mke wa kwanza wa rais kuwahi kushiriki mbio hizo.

Bi Kenyatta alishiriki mbio za London Marathon kama sehemu ya mradi wake wa kuchangisha pesa za kuwasaidia wanawake wajawazito kujifungua katika mazingira salama na kuhakikisha kuwa watoto wao pia wanaishi nchini Kenya.

Lengo lake kuu ni kupunguza idadi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga.

Wanawake wengi na watoto wachanga nchini Kenya hupoteza maisha yao wakati wa kujifungua kutokana na ukosefu wa huduma salama na sasa mama Kenyatta amejitwika jukumu la kuwapa akina mama wajawazito uwezo wa kujifungua salama.

Bi Kenyatta alikuwa na kikundi cha wasaidizi 8 waliokuwa naye hadi alipofika mwishoni mwa mbio hizo.

Wakenya kutoka sehemu mbali mbali Uingereza walifika mjini London kushuhudia Bi Kenyatta akikamilisha mbio hizo.

Wakenya ndio walioshinda mbio hizo upande wa wanawake na wanaume.

Wilson Kipsang aling'aa upande wa wanaume kwa kuweka rekodi mpya ya saa mbili na dakika nne. Kipsang alifuatiwa na mkenya mwenzake Stanley Biwott.

Kwa upande wa wanawake, Edna Kiplagat alishikilia nafasi ya kwanza akifuatiwa na mkenya mwenzake Florence Kiplagat

Italy ex-PM Berlusconi to do community service - court

Silvio Berlusconi - file pic Silvio Berlusconi has been fighting court battles for years


Italy's former Prime Minister Silvio Berlusconi must do one year's community service over tax fraud, a Milan court has ruled.

He was convicted of tax fraud in connection with TV rights purchased by his firm Mediaset.

The alternative to community service had been house arrest. It is not yet clear what form his community service will take.

The billionaire has been embroiled in a string of court cases

IKULU YAMALIZA UTATA WA HATI YA MUUNGANO

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj2xItm8S-LwHv4mAif7-7NcL7NszxkYW5JpwnGpfY28uNAIHQwoICosub-ao5f2V_VpUTm_rLX8h_UisbLbAsC10J9OLivFmIGlaqrD3ctYguyM4eFYSUXkcbT52JizXQrVcft7LAjzG1y/s1600/D92A5088.jpg

Balozi Sefue akionesha Hati ya Muungano.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiowaonesha waandishi wa habari hati halisi ya Muungano ikulu jijini Dar es Salaam leo jioni (picha na Freddy Maro)


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEifV_K0N9pUx6-Fd2QDfiG6yyL9m_O4hK-p8eyMTFKwVmpVsRzJjNZUZlCzlu0KrY_rRRiO-NA92aE1QCnoNv02MGXZ8sBdJ-NBb-VawN-sGmrrWY5tb7pNkTg2vQ_zKVTYICT6gqjfO9Bf/s1600/D92A5126.jpg
Hii ni sehemu ya Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS


Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.


TAMKO LA KATIBU MKUU KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 14 APRILI, 2014
______________________________ ____________________
Siku 12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.


Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles of the Union).


Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.

Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.


Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.


Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungia ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile.

Lakini sasa maneno yanakuwa mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.


Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.


Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.


Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione.


Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo Watanzania wenzetu, wafikie hapo.
Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.


Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.


Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
DAR ES SALAAM.