SERIKALI imemuondoa katika nafasi yake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Misitu Tanzania (TFS), Gerald Kamwenda na wakurugenzi wenzake, katika
jitihada za kufumua na kusuka upya shirika hilo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ametangaza
hatua hiyo ya serikali jana alipokutana na vyombo vya habari na kuongeza
kuwa, watumishi wengine 41 wamehamishwa vituo vya kazi.
Alifafanua kuwa hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lililotaka kufumuliwa na kusukwa upya kwa
TFS ili kuongeza ufanisi.
Kutokana na hatua hiyo, Waziri Maghembe alisema Profesa Dos Santos
Silayo ameteuliwa kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, wakati Kamwenda
anahamishiwa Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi.
Aidha, Mwanaidi Kijazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Raslimali
za Misitu na Nyuki, yeye amekwenda kuwa Mhifadhi Mkuu Amani Nature
Reserve na nafasi yake inachukuliwa na Zawadi Mbwambo.
Waziri Maghembe alisema Mohamed Kilongo aliyesimamishwa kazi Januari
5, mwaka huu uchunguzi umeonekana hana hatia na hivyo anaendelea kuwa
Mkurugenzi Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu.
Alisema Wizara imeamua Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki,
Gladnes Mkamba ahamishiwe Idara ya Mipango makao makuu na nafasi hiyo
kuteuliwa Dk Ezekiel Mwakalukwa, kuwa Kaimu Mkurugenzi.
Aidha Monica Kagya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo
ya Ufugaji Nyuki, anakuwa Mtafiti Mwandamizi Idara ya Nyuki (Tawiri).
Alisema Kagya ni mtaalamu wa masuala ya nyuki, hivyo atahamishiwa
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, ili ashughulikie utafiti wa masuala
ya nyuki.
Pia alisema katika Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa
anakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, nafasi ambayo ilikuwa
ikishikiliwa na Herman Kerayo ambaye anahamishiwa Idara ya Mipango Makao
Makuu.
Profesa Ramadhan Kideghesho, yeye anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha
Mweka wakati Mabula Misungwi aliyekuwa Meneja Mradi Selous, anakwenda
Chuo cha Wanyamapori Pasiansi na nafasi yake inachukuliwa na Jaffary
Lyimo, huku Robert Mande akipelekwa kuwa Kaimu Mkurugenzi msaidizi
Uzuiaji Ujangili.
Waziri Maghembe alisema Majjid Ally ameteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa
Kitengo cha Leseni, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Haji Mpya ambaye
amehamishiwa Shamba Jipya Songea kuwa Ofisa Misitu Alisema Julai 18,
mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikutana na viongozi na
watumishi wa Wizara hiyo na watendaji wakuu na watumishi wa TFS na
kuagiza kufumuliwa na kusukwa upya kwa wakala huo.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alitaka kuondolewa kwa utitiri wa
vituo vya ukaguzi na kuwekwa vituo vichache na kuondolewa kwa ofisi za
makontena yanayotumiwa na ofisi ya TFS, badala yake watumishi wanaofanya
ukaguzi wasimame mahali pa wazi ili kuondoa mianya ya rushwa na kuweka
uwazi katika utendaji.
- Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
-
Imechapishwa: 23 Julai 2016