Bunge la chini nchini Uholanzi limeidhinisha kuhalalishwa kwa kilimo cha bangi.
Mswada huo ulioidhinishwa, utawakinga wakulima wa bangi ambao wanatimiza masharti fulani dhidi ya kuadhibiwa.Muswada huo bado haujaidhinishwa kuwa sheria, kwani utahitaji pia kuungwa mkono na Bunge la Seneti.
Ununuzi wa viwango vidogo vya bangi katika 'migahawa' unakubalika nchini Uholanzi.
Hata hivyo upanaji wa mmea huo na kuuzia kwa wingi migahawa ni kinyume cha sheria.
Migahawa hiyo hulazimika sana kununua bangi kutoka kwa walanguzi.
Mswada huo wa Jumanne ulifikishwa bungeni na mbunge wa chama chenye msimamo wa kutetea uhuru wa raia cha D66, ambacho kwa muda mrefu kimetetea kuelegezwa kwa masharti kuhusu kilimo cha bangi.
Mswada huo uliungwa mkono na wabunge 77 dhidi ya 72, licha ya mwendesha mashtaka wa umma kueleza wasiwasi kwamba kuhalalisha kilimo cha bangi kutaifanya Uholanzi kukiuka sheria za kimataifa.
Wizara ya Afya pia ilikosoa muswada huo.
Hata hivyo, wengi wanasema huenda ikawa vigumu kwa muswada huo kupitishwa katika Seneti, iwapo maseneta watapiga kura kwa msingi wa vyama.
Lakini licha ya shaka kuhusu hatima ya muswada huo, wadau katika sekta ya bangi wamesema wamefurahishwa na ufanisi huo.
"Ni habari njema kwa sekta ya migahawa kwani hatimaye - iwapo itapitishwa na Bunge la Seneti - itafikisha kikomo mambo mengi ambayo hatuwezi kuyafanya kwa mpangilio na kwa uwazi," Joachim Helms, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Migahawa, aliliambia shirika la habari la Associated Press.