Mfalme wa Saudi Arabia Abdullah bin Abdul-Aziz Al Saud alifariki dunia 
siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 90, na kurithiwa na na mdogo wake 
Salman, kama mtawala wa juu kabisaa wa taifa hilo tajiri wa mafuta.
Viongozi wa ulimwengu wametuma salaam za rambirambi kufuatia kifo cha 
Mfalme Abdullah, anaeangaliwa kama mwanamageuzi mwenye tahadhari, 
alieliongoza taifa hilo la kifalme katika kipindi cha misukosuko, katika
 kanda iliyotikiswa na joto la mageuzi katika mataifa kadhaa ya Kiarabu 
na itikadi kali za dini ya Kiislamu.
Ofisi ya Kifalme haikutaja sababu ya kifo cha Abdullah, lakini alilazwa 
hospitali mwezi Desemba akisumbuliwa na homa ya mapafu, na alikuwa 
akipumua kwa msaada wa mashine.
Chini ya utawala wake ulioanza mwaka 2005, Saudi Arabia imekuwa mshirika
 muhimu wa utawala mjini Washington katika ulimwengu wa Kiarabu, 
ushirika wa karibuni zaidi ukiwa wa muungano wa mashambulizi dhidi ya 
kundi la Dola ya Kiilsamu nchini Iraq na Syria, unaoongozwa na Marekani.
Rais wa Marekani Barack Obama amemueleza Abdullah kama mshirika 
anaethaminiwa. Salaam nyingine za rambirambi zimetoka Japan, India, 
Ufilipino, Pakistana na Ufaransa na pia kutoka kwa katibu mkuu wa Umoja 
wa Mataifa Ban Ki-moon.
 
Mfalme mpya Salman bin Abdul-Aziz.
 
Kifo chake chapandisha bei za mafuta
Kama taifa linaloongoza kwa uzalishaji mafuta duniani, Saudi Arabia 
imechangia pakubwa uamuzi wa OPEC kukataa kupunguza uzalishaji ili 
kusaidia bezi za mafuta, ambazo zimeshuka kwa zaidi ya asilmia 50 tangu 
mwezi Juni. Bei za nisahti hiyo zilipanda leo, kufuatia kifo cha 
Abdullah, kukiwa na wasiwasi juu y aiwapo mfalme mpya Salman bin 
Abdul-Aziz ataendeleza sera hiyo.
Lakini Salma amesema katika hotuba yake kwa njia ya Televisheni muda 
mfupi uliyopita, mflame huyo mpya mwenye umri wa miaka 79 ameahidi 
kuendeleza sera za watangulizi wake. "Tutaendelea kuziheshimu sera 
sahihi ambazo Saudi Arabia imezifuata tangu kuasisiwa kwake," alisema 
mfalme huyo.
Abdullah alifanya mageuzi ya tahdhari wakati akiwa madarakani, 
akiwapinga wahafidhina kwa hatua kama vile kuwajumlisha wanawake katika 
baraza la ushauri maarufu kama Shura. Aliongoza maendeleo ya kiuchumi ya
 falme hiyo, na alisimamia mchakato wa nchi kujiunga na shirika la 
biashara duniano WTO, akitumia fedha za mafuta kujenga miji mipya ya 
kiuchumi, vyuo vikuu na njia za reli.
Lakini Saudi Arabia bado inakosolewa kwa rekodi yake ya haki za 
binaadamu, ikiwemo kufungwa kwa wapinzani. Pia ndiyo nchi pekee duniani,
 ambako wanawake hawaruhusiwi kuendesha magari.
 
Mfalme Abdullah enzi za uhai wake.
 
Mkereketwa wa familia ya kifalme
Salman ni mkereketwa wa familia ya kifalme anayesifiwa kwa kuubadili mji
 wa Riyadh wakati wa kipindi cha nusu karne alichokuwa gavana wake. 
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wasiwasi juu ya afya yake, 
baada ya kufanyiwa upasuaji mgongoni, lakini Salman alichukuwa jukumu 
kubwa zaidi pale matatizo ya kiafya ya Abdullah yalipomlaazimu kukaa 
pembeni.
Salman pia ameshikilia nyadhifa za waziri wa ulinzi na mambo ya ndani, 
na alikuwa sehemu muhimu ya diplomasia ya Saudi Arabia, akizitembelea 
mara kwa mara nchi za Magharibi. Mwaka uliyopita alifanya ziara yake ya 
kwanza nchini China na mataifa mengine ya Asia, katika hatua ilioonekana
 kama jaribio la kuelekea mashariki.
Changamoto zinazomkabili
Mfalme Abdullah alimteuwa Murqim kama naibu mrithi wa kiti cha ufalme 
mwezi Machi mwaka jana, katika hatua ya kihistoria iliolenga kurahisha 
mchakato wa urithi. Murqim, ambaye ni mkuu w azamani wa idara ya 
ujasusi, alikuwa mtu wa karibu sana wa Abdullah akiwa na sifa ya 
uliberali.
Afisa huyo wa zamani wa jeshi la anga aliezaliwa mwaka 1945, ndiye mtoto
 wa mwisho wa Mfalme Abdul-Aziz bin Saud, mwasisi wa taifa la Saudi 
Arabia. Tangu kifo cha Mfalme Abdul-Aziz mwaka 1952, kiti cha ufalme 
kimekuwa kikirithiwa na watoto wake. Abdul-Aziz alikuwa watoto 45 
waliorekodiwa na Abdullah, Salman na Murqim walizaliwa kwa mama tofauti.

Marehemu Abdullah akiwa ndani ya Swala na baadhi ya wanafamilia wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia.
 
Mfalme mpya atakabiliwa na changamoto kubwa, hasa wakati ambapo kushuka 
kwa bei za mafuta kunapunguza mapato ya taifa. Saudi Arabia imeweza 
kuepuka machafuko yaliyoyatikisa mataifa mengi ya Kiarabu katika miaka 
ya hivi karibuni, kutokana na matumizi makubwa ya umma.
Taifa hilo limejiwekea akiba ya fedha, lakini tayari limetabiri nakisi 
ya dola bilioni 38.6 mwaka huu. Wasaudia wengi walitumia mitandao ya 
kijamii kuomboleza kifo cha mfalme wao.
Tayari Salma amemteuwa mwanaye Mohammed bin Salman kuwa waziri wa ulinzi
 na mkuu wa ofisi ya Kifalme, huku mawaziri wengine wakibakia katika 
nyafisha zao, huku akimtangaza mjukuu wa muasisi wa taifa hilo Mohammed 
bin Nayef kuwa naibu mrithi wa kiti cha ufalme.