Na Mwandishi Wetu, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele, amejiuzulu wadhifa wake, huku akiwa na siri nzito.
Mnyele ambaye kitaaluma ni mwanasheria msomi, amejiuzulu jana huku
akiwa amedumu katika wadhifa huo kwa miezi minane tangu ateuliwe na Rais
Dk. John Magufuli.
Hata hivyo hakuweka wazi sababu za kujiuzulu kwake.
Taarifa zinaeleza kuwa, jana Mnyele alikutana na Kamati ya Madiwani
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuwaaga rasmi kuwa yeye si mtumishi
tena wa Serikali.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, Said Ntahoni ambaye alihudhuria kikao cha madiwani wa Wilaya ya
Uyui, alikiri kujiuzulu kwa Mnyele na kusema ameacha pengo kubwa katika
wilaya hiyo.
“Ni kweli amejiuzulu nafasi hii tangu jana, amekuja mbele ya Kamati
ya Madiwani CCM Wilaya, akatwambia amejiuzulu nafasi yake, japo hakuweka
wazi sababu za kuchukua uamuzi huo.
“Aliwaambia wajumbe kwamba amemwandikia barua Rais Magufuli na
ameridhia aachie ngazi…wajumbe wengi walibaki wameduwaa kwa sababu yeye
ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya yetu… kwa kuwa
ni uamuzi wake hatukuwa na namna tena.
“Tumekuwa naye kwa miezi nane hapa, ametusaidia katika mambo mengi,
nguvu yake ilikuwa bado inahitajika kwa wanaUyui ambao amekuwa akifanya
nao kazi za kila siku,” alisema Ntahoni.
Alisema pengo la Mnyele ni kubwa, lakini anaamini Rais Magufuli
atawapelekea kiongozi mwingine mchapakazi ambaye watashirikiana nae kwa
kila nyanja ili kuinua maendeleo ya wilaya hiyo.
MNYELE
MTANZANIA ilimtafuta DC Mnyele na alipoulizwa iwapo amejiuzulu nafasi
yake, alianza kwa kusema. “Ndo nasikia kwako niko ofisini kwangu
naendelea kuchapa kazi niliyotumwa na mamlaka za uteuzi.
“…unajua unapoteuliwa unatangazwa, unapotumbuliwa unatangazwa sasa taarifa hizo wewe umezitoa wapi?
“Ukitaka kujua suala hili, sehemu nzuri na ‘source’ wa uhakika mtafute
Gerson Msigwa (Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu), anajua ‘issue’ (suala)
hili,” alisema Mnyele.
Hata hivyo Msigwa alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema
hajapata taarifa zozote kutoka mamlaka zinazohusika juu ya kiongozi huyo
kujiuzulu.
Wakati ikiwa haijulikani sababu za kujiuzulu kwake, taarifa nyingine
zinasema Mnyele amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni
kutokana na kutingwa na majukumu yake binafsi aliyonayo.
Chanzo chetu cha uhakika, kinasema Mnyele aliandika barua ya kuomba
kijiuzulu mwaka jana, kwa Rais Magufuli ambayo ombi lake limekubaliwa na
amejibiwa juzi.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ambao hawakutaka kutajwa
majina yao, waliiambia MTANZANIA kuwa jana asubuhi Mnyele alipita kila
idara akianzia ofisini kwake kuaga wafanyakazi, huku akionekana kuwa ni
mwenye furaha.
“Bosi wetu alianzia ofisini kwake kuaga watumishi, baadae alipita
kila idara na kubwa ambalo alikuwa akieleza ni uamuzi ambao ameufanya
yeye mwenyewe bila shinikizo.
“Bosi wetu kasema uamuzi wa kusitisha ajira yake hautokani na
kushindwa kwendana na kasi ya Rais Dk. Magufuli, bali anataka kufanya
kazi zake
binafsi,” alisema mmoja wa watumishi wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo (DED), Hadija Makuwani
alisema yeye ni miongozi mwa watu walioagwa jana asubuhi na mkuu huyo wa
wilaya.
Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ili kuzungumzia
suala hilo, hazikufanikiwa kutokana na kuwa wilayani Nzega kwa shughuli
ya ukaguzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.
CHANZO MTANZANIA