Muungano huo umesema umefikia uamuzi wa kusimamisha mashambulizi hayo ya
anga ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki nne sasa, baada ya kutimiza
malengo yake ya kijeshi, ya kuondoa kitisho cha usalama wa Saudi Arabia
na nchi nyingine majirani.
Umesema sasa unageukia mchakato wa kisiasa kujaribu kuusuluhisha mgogoro
wa Yemen, na kuongeza kuwa uwezekano wa kuanza upya kwa mashambulizi
hayo unaachwa wazi, ikiwa hali italazimu hivyo. Vile vile, kulingana na
tangazo la muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia, mzingiri wa bahari
na anga utaendelea dhidi ya Yemen, ambayo iko katika eneo la kimkakati
katika Mashariki ya Kati.
Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia Brigedia Jenerali Ahmed Asiri amesema
uamuzi huo umefuatia ombi la rais wa Yemen. Abd-Rabo Mansour Hadi
aliyeko ukimbizini nchini Saudi Arabia.
Msemaji wa jeshi la Saudi Arabia, Brigedia Jenerali Ahmed Asiri
Amesema, ''Leo uongozi wa muungano umeamua kusimamisha
operesheni ''Dhoruba Kabambe'' kufuatia maombi ya rais wa Yemen, ambaye
anaamini malengo makuu ya operesheni hiyo yametimia, kitisho kwa watu wa
Yemen kimeondolewa, na waasi wa kihouthi wamepoteza uwezo wa kuwatisha
watu wa Yemen na jirani zao. Serikali ya Yemen itachukua hatua
kuwarejeshea matumaini watu wa nchi hiyo''.
Bado wahouthi wanashika hatamu
Hata hivyo licha ya madai hayo ya mafanikio, waasi wa kihouthi bado
wanaudhibiti mjini mkuu wa Yemen, Sanaa, na rais Abd-Rabo Mansour Hadi
bado yuko ukimbizini nchini Saudi Arabia. Hali kadhalika mapambano
makali yanaendelea katika mji wa bandari wa Aden.
Iran, taifa la kishia ambalo linashutumiwa kuwaunga mkono wahouthi,
imeukaribisha uamuzi huo wa kusitisha mashambulizi, ikisema ni hatua
nzuri inayofungua mlango kwa njia za kisiasa kuusuluhisha mzozo wa
Yemen.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema hatua hiyo
haina budi kufuatiwa na msaada wa kibinadamu na mjadala miongoni mwa
wayemen na serikali yenye kushirikisha makundi yetu. ''Tuko tayari
kusaidia'', amesema waziri huyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa
Twitter.
Marekani yapeleka meli za kivita
Marekani yajizatiti kuweza kuizuia Iran kupeleka silaha Yemen
Marekani pia imesema imelipokea vyema tangazo hilo la
kusimamisha mashambulizi dhidi ya wahouthi, na kutoa rai ya kufanyika
haraka mazungumzo ili kuepusha mvutano baina ya mataifa yenye ushawishi
katika ukanda huo.
Hata hivyo Marekani imetuma meli yake ya kubeba ndege za kivita USS
Theodore Roosevelt, ikisindikizwa na nyingine ya kubeba makombora USS
Normandy, kukiwa na ripoti kwamba msafara wa meli tisa za Iran zimeng'oa
nanga na kuanza safari baharini.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Kanali Steven Warren amesema
meli za Marekani zilikuwa zikijiandaa kuuzuia msafara huo wa Iran, ikiwa
utakuwa umebeba silaha.
Waasi wa kihouthi wameitisha maandamano makubwa mjini Sanaa leo,
kuadhimishwa kusitishwa kwa mashambulizi ya Saudi Arabia na washirka
wake.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo